RC RUVUMA AIAGIZA KAMPUNI YA MANTRA KUSHIRIKIANA NA TFS UPANDAJI WA MITI

Meneja wa Shamba la Miti Wino lililopo kata ya Wino Halmashauri ya Madaba linalomilikiwa na wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)Glory Kasmir kulia,akimueleza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge hatua inayoendelea ya kupanda miti katika maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na shughuli za kibidamu katika mkoa huo wakati wa uzinduzi wa mpango wa upandaji miti kimkoa uliofanyika katika kata ya Mateteleka.

***************

Na Cresensia Kapinga na Stephano Mango,Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbat Ibuge ameitaka Kampuni ya uchimbaji wa Madini aina ya URANIUM  yaliyopo mto mkuju Wilayani Namtumbo( Mantra) Tanzania Rosatom kushirikiana na Wakala wa huduma za  Misitu Nchini(TFS) ili wawashauri kuhusiana na miti inayofaa kupandwa kulingana na eneo husika

Wito huo umetolewa jana wakati alipotembelea maonesho ya banda la Kampuni ya Mantra, pamoja na  banda la TFS wakati wa ufunguzi wa wiki ya Tamasha la Kumbukizi ya Vita vya Majimaji linalofanyika kila mwaka kuanzia February 23 hadi February 27  kwenye viwanja vya makumbusho hayo.

Mkuu wa Mkoa Ibuge alisema kuwa Serikali ipo kwenye mpango wan chi nzima ya kupanda miti kitaifa angalau milioni 1.5 kwa mwaka, hivyo kutaondoka kwenye upandaji wa kizamani wa kila mtu anapanda miti kiholela bila kujali eneo la pale anapokwenda kupanda miti  kama linastahili na si vinginevyo.

“Mtazamo wa Serikali kwa sasa ni kupanda miti kitaalamu ili kupunguza hewa ya ukaa kwasababu ni ajenda ya kitaifa na ili tuwe na upandaji endelevu wa miti hiyo kwa lengo la kutunza mazingira na vyanzo vya maji ni lazima wakala wa huduma za Misitu (TFS) wahusike ili kushauri aina ya miti inayofaa kupandwa kulingana na eneo husika” Alisema Ibuge

Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Ibuge kwenye banda la kampuni ya Mantra Afisa Uhusiano wa Kampuni hiyo Khadija Palangyo alisema kuwa kampuni imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upandaji wa miti kwa kushirikiana na idara ya mazingira (NEMC) na kwamba maelekezo yote ambayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa ameyapokea na atayafikisha eneo husika ili yaweze kufanyiwa kazi.

Awali Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Kusini Manyisye Mpokigwa alimwambia Mkuu wa Mkoa kuwa Wakala inashughulika na uhifadhi wa misitu asilia pia inajihusisha na ufugaji wa nyuki ambao hauhathiri mazingira

Mpokigwa alisema kuwa idara ya misitu na nyuki inajihusisha zaidi na ufugaji wa nyuki kisasa na upatikanaji wa asali, ambapo idara ya misitu inajihusisha na shughuli za kila siku za kuendeleza misitu iliyohifadhiwa kitaifa na misitu ya kupandwa ambayo itakuwa kivutio cha utalii.

Naye Mhifadhi Mkuu Shamba la miti Sao  Hill Lucas Sabida alisema kuwa tunawaelimisha wananchi namna ya upandaji wa miti kisasa na uhifadhi wa miti hiyo kwa lengo la utunzaji wa mazingira,vyanzo vya maji pamoja  na kibiashara.

Post a Comment

0 Comments