Waziri Simbachawene Aweka Mkakati wa Kuliboresha Jeshi la Magereza kwa Teknolojia ya Kilimo

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ameweka wazi dhamira ya Serikali ya kuunganisha nguvu kazi ya wafungwa na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kilimo, ili Jeshi la Magereza liendane na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha tija katika shughuli za kilimo zinazofanyika magerezani, sambamba na kuhusisha sekta binafsi katika uzalishaji.

Kauli hiyo imetolewa leo wakati wa ziara ya kukagua shughuli za kilimo, ikiwemo shamba la mahindi katika Gereza la Kilimo na Mifugo la Kitengule, wilayani Karagwe mkoani Kagera. Waziri Simbachawene amesisitiza umuhimu wa Jeshi la Magereza kubadili mtazamo na kuendana na maendeleo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia mbegu bora, teknolojia ya kisasa na mashine kubwa za kilimo.

“Lazima twende kwenye mabadiliko. Tutashirikiana na SHIMA (Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza) kuhakikisha tunaingia kwenye kilimo cha kisasa kinachotumia mashine kubwa ili kuzalisha kwa wingi. Kimsingi tuna fursa ya kuilisha nchi nzima, si kuishia kuwalisha wafungwa pekee. Tuna maeneo makubwa ya kilimo, tutashirikisha sekta binafsi kupitia SHIMA, na pia tunaelekea kwenye kilimo cha kidijitali kitakachotuwezesha kulima maeneo makubwa kwa tija zaidi. Nafahamu jitihada zilishaanzishwa na wenzangu, nami natarajia kuendelea pale walipoishia,” amesema Waziri Simbachawene.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya kilimo na mifugo, Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Mikael Mafwele, amesema lengo lao ni kuongeza uzalishaji licha ya changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo, ikiwemo upungufu wa mvua na uwepo wa wanyama waharibifu wa mazao kama nguruwe pori na nyani.

“Kwa ujumla tuna ekari 200, lakini tumelima ekari 160. Changamoto kubwa imekuwa ni uchelewaji wa mvua ya kutosha, hali inayolazimu kulima eneo dogo. Pia tunakabiliwa na wanyama waharibifu wa mazao, lakini tunaendelea kuimarisha ulinzi ili kukabiliana na changamoto hiyo,” amesema ACP Mafwele.

Post a Comment

0 Comments