Salome Makamba:Rukwa kupata umeme wa gridi Mei 2026

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanatarajiwa kuanza kupata umeme wa gridi ya taifa kuanzia mwezi Mei mwaka 2026 mara baada ya kukamilika kwa mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka mkoani Iringa.

Amesema hayo katika Mji wa Laela wakati wa ziara ya Mwigulu Nchemba mkoani Rukwa Region.

Makamba amesema kuwa kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, serikali inaendelea kuhakikisha kuwa ifikapo Mei 2026 umeme utaanza kuwashwa kupitia mradi wa TAZA.

“Kwa sasa hali ya mradi inaendelea vizuri na kama kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa, ifikapo mwezi Mei mwaka huu hatimaye Mkoa wa Rukwa utaanza kunufaika na umeme wa gridi ya taifa,” amesema Makamba.

Ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa wa Rukwa unapata umeme kutoka nchini Zambia kupitia ushirikiano wa biashara ya umeme wa nchi za Kusini mwa Afrika chini ya mpango wa Southern African Power Pool, unaowezesha nchi wanachama kuuza au kununua umeme kulingana na mahitaji.

Aidha, amesema kuwa kutokana na nchi kuwa na umeme wa kutosha, serikali inaendelea kujenga miundombinu imara ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Makamba amesema jitihada mbalimbali zinaendelea ili kufikia lengo la asilimia 80 ya wananchi kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, ikiwa ni pamoja na kusambaza majiko banifu na mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku.

Post a Comment

0 Comments