Zanzibar:Wananchi Wataka Masoko Rasmi ya Madini

 

Wananchi wa Zanzibar wameiomba Serikali kupitia Tume ya Madini kuanzisha masoko na minada rasmi ya madini Visiwani humo ili kuwawezesha wafanyabiashara, wachimbaji wadogo na wawekezaji kufanya biashara ya madini kwa uwazi, usalama na bei shindani.

Ombi hilo limetolewa na wananchi waliotembelea Banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar yanayoendelea kufanyika Fumba, ambapo wameeleza kuwa ukosefu wa masoko rasmi na minada ya madini umekuwa kikwazo kwao kushiriki kikamilifu katika biashara ya madini.

Wamesema kuwepo kwa masoko na minada ya madini kutachochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake, kuongeza kipato kwa wananchi pamoja na kudhibiti biashara holela ya madini.

Kupitia maonesho hayo, Tume ya Madini inaonesha fursa katika utafutaji wa madini, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani, biashara ya madini pamoja na utoaji wa bidhaa na huduma kwa shughuli za migodini.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa Tume ya Madini, Greyson Mwase, amesema sekta ya madini inatoa fursa jumuishi kwa makundi yote ikiwemo wachimbaji wadogo, vijana na wanawake na kuwataka wananchi wa Zanzibar kujiandikisha na kuomba Leseni za Uchimbaji Mdogo wa Madini (PML), kushiriki katika uongezaji thamani wa madini na kutumia mifumo rasmi ya biashara ya madini.

Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar yataendelea hadi Januari 16, 2026, na wananchi wanakaribishwa kutembelea Banda la Tume ya Madini kwa ajili ya kupata elimu, ushauri na kugundua fursa za uwekezaji katika sekta ya madini inayokua kwa kasi nchini.

Post a Comment

0 Comments