Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imewachagua wanafunzi 145 wenye ulemavu na mahitaji maalum kujiunga na vyuo vya VETA kwa mwaka wa masomo 2026, hatua inayolenga kukuza usawa, ujumuishi na upatikanaji wa elimu ya ufundi stadi kwa makundi yote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 23, 2025, katika Makao Makuu ya VETA jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kati ya waombaji 195 wenye mahitaji maalum walioomba kujiunga na vyuo vya VETA, wanafunzi 145 tayari wamepangiwa vyuo 53 huku waombaji 50 wakiendelea kusubiri kupangiwa.
CPA Kasore amesema waombaji hao wanajumuisha watu wenye changamoto za uoni, usikivu pamoja na ulemavu wa viungo, na kubainisha kuwa serikali imeamua kugharamia ada za mafunzo kwa waombaji wote 195 kuanzia ngazi ya kwanza hadi ya pili ili kuondoa changamoto za kifedha.
Ameeleza kuwa zoezi la uchaguzi wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2026 limefanyika kwa kuzingatia miongozo ya serikali na kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETMIS), jambo lililosaidia kuongeza uwazi na ufanisi.
Kwa mujibu wa CPA Kasore, jumla ya waombaji 18,875 walijitokeza kuomba kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA mwaka huu, ambapo wanawake walikuwa 6,915 sawa na asilimia 37 na wanaume 11,960 sawa na asilimia 63.
Ameongeza kuwa katika mchakato wa upangaji wa wanafunzi, VETA imezingatia vigezo mbalimbali ikiwemo historia ya maombi ya awali, uwezo wa kila chuo, ulinganifu wa fani zilizoombwa, pamoja na kutoa kipaumbele kwa wanawake na waombaji wenye mahitaji maalum.
Akizungumzia matokeo ya jumla, CPA Kasore amesema waombaji 14,433 sawa na asilimia 76 wamefanikiwa kupangiwa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ngazi ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2026. Kati yao, wanaume ni 8,776 sawa na asilimia 61 na wanawake ni 5,657 sawa na asilimia 39.
Amebainisha kuwa kati ya waliochaguliwa, waombaji 12,942 wamepangiwa masomo ya asubuhi, huku 1,491 wakipangiwa masomo ya jioni. Aidha, waombaji 4,511 sawa na asilimia 24 bado wanasubiri kupangiwa vyuo na fani mbadala kutokana na kuchagua fani moja au kukosa kuchagua fani mbadala.
CPA Kasore amesema mafunzo hayo yanatolewa katika jumla ya fani 45, ambapo fani ya Umeme imeongoza kwa kuwa na waombaji 2,980 sawa na asilimia 20.65. Kwa upande mwingine, fani za Useketaji (Handloom Weaving) na Uendeshaji wa Mitambo (Plant Operation) ndizo zilizopata
waombaji wachache zaidi, kila moja ikiwa na waombaji watatu.
Katika kundi la waombaji wenye elimu ya juu, CPA Kasore amesema VETA imepokea waombaji 134 wenye Astashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili, ambapo 123 wamechaguliwa na 11 wanasubiri kupangiwa. Amesema baadhi ya masomo ya msingi kwa kundi hilo yameondolewa ili kupunguza muda wa mafunzo na kuongeza ufanisi.
Aidha, amesema VETA imeondoa Mtihani wa Mchujo (Aptitude Test) katika udahili, hatua inayolenga kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi bila vikwazo.
Kwa kuongeza wigo wa mafunzo, VETA pia imeanzisha masomo ya jioni katika vyuo 13, ambapo waombaji 1,491 wanatarajiwa kuanza masomo Januari 2026, ili kuwahudumia wale wenye majukumu ya kazi au shughuli nyingine wakati wa mchana.



0 Comments