Kwagilwa Aagiza Kukamatwa Mkandarasi na Mhandisi wa Mradi wa Barabara Ilala

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Reuben Kwagilwa, ametoa agizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala kuwakamata na kuwahoji Mkandarasi pamoja na Mhandisi Mshauri wa mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kitunda–Kivule–Msongola, kutokana na ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi huo.

Agizo hilo limetolewa baada ya Naibu Waziri huyo kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, unaogharimu Shilingi bilioni 30.37 na kutekelezwa na Kampuni ya Jiangxi Geo Engineering Co. Ltd, huku Mhandisi Mshauri akiwa ni Mhandisi Consultancy Ltd. Hadi sasa, Serikali tayari imelipa Shilingi bilioni 4 kwa mkandarasi huyo.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mhe. Kwagilwa amesema Serikali haitavumilia uzembe wala kutotekelezwa kwa miradi kwa mujibu wa mikataba, akisisitiza kuwa mradi huo ni wa muhimu kwa maisha ya wananchi na maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam.

“Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, ninamuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kuhojiwa mara moja. Wanapaswa kuwasilisha mpango wa haraka wa utekelezaji. Hakuna nyongeza ya muda; ifikapo Aprili mradi huu lazima uwe umekamilika,” amesema.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara yenye jumla ya kilomita 12.74, ikijumuisha Barabara ya Kitunda–Kivule–Msongola (km 9.95) na Kivule–Majohe Junction (km 2.79), unaotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II).

Taarifa zinaonyesha kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 33 tangu ulipoanza Januari 2025, huku kukiwa na matarajio ya kukamilika Aprili 2026. Hata hivyo, Serikali imeeleza kuwa kasi hiyo hairidhishi na iko kinyume na malengo ya mradi.

Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria na kiutawala dhidi ya wakandarasi na wasimamizi wa miradi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inawanufaisha wananchi kama ilivyopangwa.

Post a Comment

0 Comments