Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Bw. Raymond Mndolwa, ametembelea mradi wa bwawa la umwagiliaji la Mkomazi lililopo Kijiji cha Manga Mtindiro, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaolenga kuinua uzalishaji wa kilimo.
Akiwa katika ziara hiyo, Bw. Mndolwa alikagua maeneo mbalimbali ya mradi na kujiridhisha na hatua ya utekelezaji iliyofikiwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora, muda na matumizi sahihi ya rasilimali zilizotengwa.
Alisema ziara hiyo imelenga kufuatilia maendeleo ya ujenzi, kusikiliza changamoto zilizopo pamoja na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa mujibu wa mpango kazi wa Serikali, akibainisha kuwa Tume itaendelea kusimamia kwa karibu hadi mradi utakapokamilika.
“Serikali imejipanga kuhakikisha miradi ya umwagiliaji inakamilika kwa wakati na kuleta tija iliyokusudiwa. Mradi huu ni miongoni mwa miradi muhimu itakayobadilisha maisha ya wakulima wa Korogwe,” alisema Bw. Mndolwa.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya kilimo na kupunguza utegemezi wa mvua, hali itakayoongeza uzalishaji na usalama wa chakula nchini.
Awali, Meneja wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Tanga, Mhandisi Leonard Someke, alisema ujenzi wa bwawa la Mkomazi umefikia asilimia 85 na unaendelea kwa kasi, huku mradi huo ukitarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 04 Februari 2026.
Mhandisi Someke alisema bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika msimu wote wa mwaka, hatua itakayowezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kipato.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Manga Mtindiro na Wilaya ya Korogwe wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya umwagiliaji, wakisema mradi wa bwawa la Mkomazi utaleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wakulima wa eneo hilo.

0 Comments