Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa onyo kwa waendeshaji wa majahazi na meli ndogo wanaofanya safari za baharini kati ya Tanga, Zanzibar na Pemba, kuzingatia kikamilifu sheria za usalama kwa kutokuzidisha abiria na mizigo kutokana na hali ya bahari kutokuwa salama kwa sasa.
Onyo hilo limetolewa na Afisa Mfawidhi na Mkaguzi Mwandamizi wa Vyombo vya Majini TASAC Mkoa wa Tanga, Captain Christopher Shalua, wakati akitoa semina maalum kwa manahodha wa majahazi yanayofanya safari kupitia ukanda wa pwani ya Mkoa wa Tanga.
Akizungumza katika semina hiyo, Captain Shalua amesema kuwa kwa sasa hali ya upepo baharini imechachamaa, hali inayoongeza hatari ya ajali za majini endapo waendeshaji wa vyombo hawatazingatia kikamilifu taratibu za usalama zilizowekwa.
Amesisitiza kuwa waendeshaji wa vyombo vidogo na meli za ukubwa wa kati wanapaswa kuhakikisha wanapakia mizigo kwa kiwango kinachoruhusiwa kulingana na vyeti vya usajili walivyopewa na mamlaka husika.
Captain Shalua ameeleza kuwa kila chombo cha majini kimeainishiwa kiwango maalum cha mzigo na idadi ya abiria kinachoruhusiwa kubebwa, na ni marufuku kwa chombo chochote kuzidisha kiwango hicho kwa sababu yoyote ile.
Aidha, amewataka waendeshaji wa meli za abiria kuhakikisha wanazingatia idadi halali ya abiria inayoruhusiwa, kama ilivyoainishwa kwenye vyeti vyao, ili kuepusha hatari kwa maisha ya wasafiri.
Kwa mujibu wa TASAC, kupakia abiria au mizigo kupita kiasi ni ukiukwaji wa sheria na kunaweza kusababisha ajali zinazoweza kuepukika endapo sheria zitazingatiwa ipasavyo.
Captain Shalua amesema TASAC itaendelea kufanya doria na ukaguzi wa mara kwa mara baharini ili kuhakikisha vyombo vyote vinafuata sheria, kanuni na taratibu za usafiri wa majini.
Ameongeza kuwa kwa kipindi hiki mamlaka hiyo itasimamia sheria kwa ukaribu zaidi, na vyombo ambavyo haviruhusiwi kisheria kubeba abiria havipaswi kufanya hivyo kwa hali yoyote.
Ameonya kuwa yeyote atakayekiuka maagizo hayo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini au adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria za usafiri wa majini.

0 Comments