Tume ya Ushindani (FCC) imesema itaendelea kusimamia kwa karibu haki za walaji, hasa katika taasisi na kampuni zinazotumia mikataba iliyoandaliwa kwa upande mmoja, ili kuhakikisha watumiaji wa huduma na bidhaa hawapati hasara kutokana na mikataba hiyo.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, alipokuwa akizungumza katika semina iliyowakutanisha wadau kutoka taasisi na kampuni zinazotumia mikataba ya upande mmoja.
Amesema FCC inaendelea kufuatilia kwa karibu mikataba hiyo ili kuhakikisha haikiuki haki za walaji katika soko.
Ngasongwa amefafanua kuwa mikataba ya upande mmoja hutumiwa na taasisi mbalimbali kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakati, lakini ni muhimu iwe chini ya uangalizi ili kuepuka matumizi yanayoweza kuwa kinyume na sheria za ushindani na ulinzi wa walaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Tusekelege Mwaikasu, amesema semina hiyo ni muhimu kwa taasisi za kifedha kwani itawasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa walaji kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika.


0 Comments