Maswali yanayoulizwa sana katika kipindi hiki kuhusu Iran ni nani hasa Ayatullah Mojtaba Husseini Khamenei na kwa nini Baraza la Wataalamu limemchagua kuongoza nchi hiyo. Ili kuelewa jambo hili, ni muhimu kwanza kufahamu utaratibu wa kisheria wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa Katiba ya Iran, kiongozi wa nchi huchaguliwa na Baraza la Wataalamu, ambalo linajumuisha wanazuoni wa kidini na wataalamu wa sheria za Kiislamu. Wanachama wa baraza hilo huchaguliwa moja kwa moja na wananchi wa Iran.
Hii ina maana kuwa wananchi huchagua kwanza wajumbe wa Baraza la Wataalamu, na baadaye wajumbe hao huwa na jukumu la kumchagua Kiongozi Mkuu wa nchi.
Katika kufanya uamuzi huo, Baraza la Wataalamu huzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo elimu, uwezo wa uongozi, uzoefu pamoja na uelewa wa masuala ya kimkakati ya taifa.
Kwa upande wa Ayatullah Mojtaba Husseini Khamenei, mambo kadhaa yametajwa kuwa sababu ya kupewa nafasi hiyo.
Kwanza ni historia yake ya kielimu katika taasisi za kidini. Mojtaba alisoma kwa muda mrefu katika vyuo vikuu vya kidini vinavyojulikana kama Hauza vilivyopo Qum, ambako wanazuoni wengi wakubwa wa dini hupata mafunzo ya juu ya kidini na kisheria.
Pili ni uelewa wake wa kina kuhusu mfumo wa utawala wa Iran. Kwa miaka mingi amekuwa akifuatilia na kujifunza kwa karibu namna maamuzi makubwa ya kisiasa na kiusalama yanavyofanyika ndani ya Jamhuri ya Kiislamu.
Tatu ni uhusiano na uelewa wake kuhusu taasisi muhimu za nchi. Inadaiwa kuwa ana uzoefu na ujuzi kuhusu taasisi za kimkakati zikiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na vyombo vingine vya usalama, hali inayompa uelewa mpana wa masuala ya ulinzi wa taifa na mazingira ya kikanda.
Sababu ya nne ni mazingira ya kisiasa na kiuchumi yanayoikabili Iran kwa sasa. Nchi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vikwazo vya kiuchumi, mashinikizo ya kimataifa pamoja na ushindani wa kikanda na vita vya taarifa kupitia vyombo vya habari na mifumo ya usalama.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa Iran inahitaji kiongozi mwenye uelewa wa kina wa misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na uwezo wa kukabiliana na changamoto mpya za dunia ya sasa.
Kwa mtazamo huo, uamuzi wa Baraza la Wataalamu kumchagua Ayatullah Mojtaba Khamenei unaelezwa na baadhi ya wachambuzi kuwa ni mwendelezo wa sera ya kimkakati ya Iran ya kulinda uhuru wake wa kisiasa na kupinga mashinikizo ya nje.
Hata hivyo, jambo muhimu ni kwamba mchakato huo umefanyika ndani ya mfumo wa kikatiba wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kupitia taasisi ambayo wajumbe wake huchaguliwa moja kwa moja na wananchi.

0 Comments