Kenya Yaanzisha Matumizi ya Kamera Kwa Maafisa wa Forodha Kupambana na Rushwa

Serikali ya Kenya imeanzisha utaratibu wa kuwavalisha kamera maafisa wa forodha na mipaka kwa lengo la kurahisisha usafiri na biashara halali pamoja na kuimarisha uwajibikaji katika utendaji wa kazi.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA), jumla ya kamera 350 tayari zimepelekwa katika maeneo mbalimbali ya mipakani ili kusaidia kufuatilia shughuli za maafisa hao wanapotekeleza majukumu yao.

Hatua hiyo inalenga kuwezesha usafiri na biashara halali katika nchi hiyo ambayo ni moja ya uchumi unaokua kwa kasi katika ukanda wa Afrika Mashariki na mwenyeji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), moja ya viwanja vyenye shughuli nyingi barani Afrika.

Mamlaka hiyo imesema kamera hizo zitasaidia kupunguza vitendo vya rushwa huku picha na sauti zitakazorekodiwa zikitarajiwa kusaidia katika kutatua migogoro au tofauti zitakazojitokeza kati ya maafisa na wasafiri au wafanyabiashara.

“Wakati kamera inafanya kazi, lazima mtu awajibike. Inaporekodi mazungumzo inaimarisha viwango vya uwajibikaji kwa kila anayehusika,” ilisema sehemu ya taarifa ya mamlaka hiyo iliyotolewa Jumanne.

Hatua hiyo inakuja wakati kukiwa na wasiwasi kuhusu vitendo vya rushwa na njama zinazodaiwa kusaidia baadhi ya watu kukwepa ulipaji kodi katika maeneo ya mipakani.

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa dhamira yake ni kuhakikisha kunakuwa na usawa, uadilifu na uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa shughuli za forodha.

Aidha, kamera hizo zimeunganishwa na mfumo wa GPS wenye uwezo wa kurekodi matukio pamoja na kurusha picha mubashara, hatua inayotarajiwa kuongeza uwazi katika utendaji wa maafisa wa mipakani.

Post a Comment

0 Comments