Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametoa wito kwa Wizara zinazohusika na Sekta ya Mazingira kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwa na mpango wa pamoja utakaowezesha uhifadhi endelevu wa mazingira.
Makamu wa Rais ametoa wito huo alipokuwa akifanya mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni; Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew; Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Festo Dugange; Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Muyungi pamoja na wataalamu kutoka wizara hizo katika kikao kilichofanyika mkoani Dodoma.
Amesema wizara hizo zinategemea kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa mazingira. Alifafanua kuwa Wizara ya Maji itaweza kufanya kazi kwa ufanisi iwapo vyanzo vya maji vitalindwa dhidi ya uharibifu. Aidha, alieleza kuwa mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia utasaidia kupunguza ukataji wa miti ovyo na hivyo kulinda misitu iliyopo.
Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa wizara hizo kuongeza juhudi ili kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika kulinda na kuhifadhi mazingira, akisisitiza kuwa nchi ina misitu ya kutosha pamoja na wataalamu wenye uwezo wa kufanikisha malengo hayo.
Amesema tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua mpango wa kukijanisha nchi pamoja na kuhamasisha mara kwa mara upandaji miti kitaifa. Alitaja pia jitihada za Rais kutumia siku yake ya kuzaliwa kuhamasisha upandaji miti nchini, hivyo kuwataka watendaji kuongeza bidii ili Tanzania iwe kinara wa uhifadhi wa mazingira.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewahimiza viongozi hao kuandaa mpango madhubuti wa kukabiliana na changamoto za kuhifadhi miti baada ya kupandwa ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa na mpango wa kitaifa wa upandaji miti unaokwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani.

0 Comments