NIDA Yaongeza Mashine na Siku za Usajili wa NIN Mbeya

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, ameongeza mashine pamoja na siku za usajili wa Vitambulisho vya Taifa katika Mkoa wa Mbeya kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi wanaojitokeza kujiandikisha kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN).

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua zoezi hilo mkoani humo, Kaji amesema ameridhishwa na mwamko mkubwa wa wananchi wanaojitokeza kujiandikisha, jambo linaloonesha kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu wa utambulisho wa Taifa katika kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa takwimu za zoezi hilo, zaidi ya wananchi 7,400 tayari wamehudumiwa ndani ya siku chache zilizopita, huku wastani wa zaidi ya wananchi 400 wakisajiliwa kila siku katika zoezi maalum la usajili.

Aidha, amewahimiza wananchi kuhakikisha wanachukua vitambulisho vyao vya Taifa vilivyokwisha chapishwa ili kuepuka kusitishwa kwa matumizi ya namba zao za utambulisho.

Kwa mujibu wa takwimu za NIDA, katika Mkoa wa Mbeya pekee zaidi ya vitambulisho 130,000 bado havijachukuliwa na wamiliki wake.

Kutokana na mwitikio huo mkubwa, Mkurugenzi Mkuu ameongeza siku 10 zaidi za usajili ili kuwapa wananchi wengi fursa ya kujiandikisha na kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa.

Pia ameagiza kuongezwa kwa watendaji katika vituo vya usajili pamoja na kuwekwa kwa viti na mahema katika maeneo ya huduma ili kupunguza adha kwa wananchi wanaosubiri kupatiwa huduma.

Post a Comment

0 Comments