Ving’ora vya tahadhari pamoja na milio ya milipuko vilisikika katika mji wa Tel Aviv nchini Israel leo mchana, hali iliyozua taharuki na kuvuruga baadhi ya safari za ndege katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Taarifa zinaeleza kuwa athari za mashambulizi hayo zimegusa pia nchi kadhaa za Ghuba ikiwemo Kuwait, United Arab Emirates, Bahrain na Saudi Arabia.
Nchini Bahrain, mamlaka zimeripoti kuwa mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na Iran yamesababisha kifo cha mwanamke mmoja. Wakati huo huo, Umoja wa Falme za Kiarabu umeripoti kuzuka kwa moto katika mji wa viwanda wa Ruwais.
Katika maendeleo mengine, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema Iran “haijaomba usitishaji vita”.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa wa Iran, Ali Larijani, amepuuzilia mbali vitisho kutoka kwa Donald Trump, akivitaja kuwa “maneno matupu”, na kuongeza kuwa Rais huyo wa Marekani anapaswa kuwa makini kwa sababu “huenda yeye mwenyewe akaangamia”.
Tukio hilo limeongeza wasiwasi wa usalama katika ukanda wa Mashariki ya Kati huku mamlaka za anga zikifuatilia kwa karibu hali ya usalama wa safari za ndege katika eneo hilo.

0 Comments