Upatikanaji wa dawa ya kulevya aina ya heroini umeendelea kuwa mgumu katika Jiji la Tanga, hali inayochangia kupungua kwa baadhi ya watumiaji huku wengine wakilazimika kutumia dawa feki au kukimbilia bangi na pombe.
Imeelezwa kuwa baadhi ya waraibu wameanza kutumia mchanganyiko wa dawa mbalimbali, ikiwemo Valium,wakiamini kuwa ni heroini halisi kutokana na uhaba wa dawa hiyo katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Daktari wa afya ya akili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo,Wallace Karata, amesema zaidi ya waraibu 1,300 wamesajiliwa tangu kuanzishwa kwa huduma ya methadone mwaka 2020, huku zaidi ya 600 wakipata huduma hiyo kila siku hospitalini hapo.
Dkt.Karata alisema hali hiyo inaonyesha mafanikio ya juhudi za kudhibiti uingizwaji na usambazaji wa dawa za kulevya mkoani humo.
Alieleza kuwa Mkoa wa Tanga unashika nafasi ya pili nchini kwa matumizi ya dawa za kulevya baada ya Dar es Salaam kwa kuzingatia uwiano wa watumiaji na idadi ya watu, Tanga inaongoza.
“Kwa sasa matumizi ya heroini yamepungua. Wapo wanaodhani wametumia heroini lakini vipimo vinaonyesha hawajatumia, kwa sababu baadhi wanatumia dawa feki zinazochanganywa na dawa nyingine,” alisema Dk. Karata.
Aliongeza kuwa tangu kuanza kwa huduma ya methadone, jumla ya waraibu 100 wamefanikiwa kuacha matumizi ya dawa za kulevya na kurejea katika maisha yao ya kawaida.
Hata hivyo, alibainisha kuwa baadhi ya waraibu hulazimika kuendelea na tiba ya methadone kwa muda mrefu, kati ya miaka mitano hadi kumi, kutegemea hali ya mgonjwa.
Kwa upande wake, Afisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Shaban Miraji, alisema katika Kanda ya Kaskazini kuna vituo vitatu vya huduma za tiba saidizi (MAT) vilivyopo katika mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Manyara una mpango wa kuanzishiwa kituo hicho hivi karibuni ili kuongeza upatikanaji wa huduma kwa waraibu.
Kwa sasa Mkoa wa Tanga una kituo cha MAT katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, huku kingine kikijengwa katika Wilaya ya Muheza ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa waraibu wanaoishi mbali na jiji.

0 Comments