Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita imewafikisha mahakamani wabunge wawili wa majimbo ya Chato Kaskazini na Chato Kusini pamoja na madiwani wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Akizungumza Machi 9, 2026, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, James Ruge, amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya uchunguzi kubaini kuwepo kwa vitendo vya ushawishi kwa kutumia rushwa katika mchakato wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi hao wanadaiwa kuwakusanya madiwani wateule 20 wa Chato katika Hoteli ya Lake Zone iliyopo jijini Mwanza na baadaye katika Hoteli ya Serengeti Palace iliyopo Katoro mkoani Geita.
Inadaiwa kuwa katika mikutano hiyo madiwani walipewa fedha, chakula na malazi kwa lengo la kuwashawishi kupiga kura za upendeleo kwa mgombea aliyependekezwa kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato.
Mbinu za Kumng’oa Mpinzani
Katika tuhuma nyingine, Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini akishirikiana na aliyekuwa Diwani mteule wa Bwongera, Bartholomeo Christian Manunga pamoja na Josephat Elias Manyenye wa Kata ya Bwera, wanadaiwa kupanga njama za kumshawishi aliyekuwa Diwani mteule wa Kata ya Muungano, Njile Charles Mboligo, kujiondoa katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti.
Inadaiwa kuwa Mboligo alipewa hongo ili ajiondoe kwenye kinyang’anyiro hicho, hatua iliyolenga kumpa ushindi wa moja kwa moja Bartholomeo Manunga katika mchakato wa uchaguzi huo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
TAKUKURU imeeleza kuwa hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa hao zimechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 (Marejeo ya mwaka 2023), kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 11 ya mwaka 2024.
Uchunguzi wa taasisi hiyo umebaini kuwa mchakato wa uchaguzi huo ndani ya chama ulitawaliwa na vitendo vya rushwa, hali iliyosababisha watuhumiwa wote kufikishwa mahakamani Machi 9, 2026.

0 Comments