Wanawake wa Mzumbe University wameadhimisha International Women's Day kwa kufanya shughuli za kijamii, ikiwemo kutembelea Kituo cha Afya Mlali kilichopo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Katika ziara hiyo, wanawake hao walikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha mazingira ya utoaji huduma katika kituo hicho. Msaada huo ulijumuisha tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 5,000 kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama.
Mbali na tanki hilo, walitoa pia vifaa tiba, sabuni za maji, vifaa vya kuwekea uchafu (dustbins), vizolea uchafu, mifagio, pampers za watoto, vitambaa vya kufutia watoto (wipes) pamoja na vinywaji kwa wagonjwa. Msaada huo ulilenga kuboresha mazingira ya huduma za afya na kuwafariji wagonjwa wanaopata matibabu katika kituo hicho.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Mzumbe University, Hawa Tundui Petro alisema chuo hicho kimekuwa kikiadhimisha siku hiyo kwa kufikia jamii zenye uhitaji.
Alisema kwa takribani miaka nane sasa chuo hicho kimekuwa kikitumia maadhimisho hayo kama fursa ya kushirikiana na jamii, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza kaulimbiu ya chuo, “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.”
Aidha, alieleza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ya International Women's Day, “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050,” inalenga kutambua mchango wa wanawake katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, siasa na uchumi.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Allen Mushi aliwataka wanawake kuendelea kushirikiana na kusaidiana katika jamii huku akisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo, Elizabeth Lulu Genda alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali na kuimarisha maisha ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya kituo hicho, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mlali, Celestine Luzinga aliwashukuru wanawake wa chuo hicho kwa msaada walioutoa, akisema vifaa hivyo pamoja na tanki la maji vitasaidia kuimarisha mazingira ya utoaji huduma na kuongeza ufanisi kwa watumishi wa afya.
Baadhi ya akina mama waliopokea msaada huo walieleza shukrani zao wakisema msaada huo umeleta faraja na kuonyesha upendo mkubwa kwa jamii.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni mfano wa juhudi za wanawake wa Mzumbe University katika kushirikiana na jamii, kusaidia wenye uhitaji na kuimarisha mshikamano pamoja na usawa wa kijinsia.
.jpeg)

.jpeg)

0 Comments