Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kila taifa kujenga mfumo wa demokrasia unaoakisi utamaduni, historia na mazingira yake, badala ya kuiga mifumo kutoka nje. Akinukuu mawazo ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere, alieleza kuwa demokrasia haiwezi kuletwa kama bidhaa bali hujengwa ndani ya jamii husika.
Ameeleza kuwa Tanzania inapaswa kuendelea kuijenga demokrasia yake kwa misingi yake yenyewe. Kupitia falsafa ya 4R, amesema alianzisha majadiliano na wadau wa siasa, hatua iliyochangia kufanyika kwa marekebisho ya baadhi ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa. Sambamba na hilo, ameeleza kuwa kumekuwepo na upanuzi wa shughuli za kisiasa pamoja na kuimarika kwa uhuru wa vyombo vya habari.
Akizungumza Aprili 23, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema tangu uhuru na baada ya Muungano, Tanzania ilichagua mfumo wa demokrasia, na mwaka 1992 ikaingia rasmi katika mfumo wa vyama vingi. Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, demokrasia inapaswa kuendelezwa kulingana na mazingira ya nchi husika badala ya kuiga mifumo ya nje.
Aidha, amesisitiza kuwa amani ni rahisi kupotea lakini si rahisi kurejeshwa, huku akibainisha kuwa kubomoa nchi ni jambo jepesi kuliko kuijenga. Ameeleza kuwa changamoto za maendeleo haziepukiki, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kuzitatua badala ya kuzifanya kuwa chanzo cha vurugu na uhalifu.
Pia amesema matukio yaliyotokea hayakuondoa changamoto zilizokuwepo bali yalizidisha, na hivyo kuhimiza Watanzania kuendelea kulinda amani na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa. Ameongeza kuwa nguvu ya taifa ipo kwa wananchi wake, na hakuna msaada wa nje utakaoweza kusaidia ikiwa misingi ya ndani itaharibiwa.
Kwa upande mwingine, amebainisha kuwa baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025, kulisambaa taarifa mbalimbali zisizo sahihi, ikiwemo takwimu za vifo ambazo hazikuthibitishwa. Amesema baadhi ya taarifa hizo zilikuwa na lengo la kupunguza au kupotosha ukubwa wa madhara yaliyotokea.
Hata hivyo, amesema Tume ya uchunguzi tayari imewasilisha takwimu sahihi baada ya kufanya uchambuzi wa kitaalamu, zikionyesha idadi halisi ya waliopoteza maisha, waliojeruhiwa na waliopata madhara mengine. Ameongeza kuwa madai ya wananchi kuhusu ndugu zao kutoweka yataendelea kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wake.


0 Comments