Ripoti Yaweka Wazi Sababu za Ghasia za Baada ya Uchaguzi Mkuu

Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande, amesema ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu zilichangiwa na mchanganyiko wa matatizo ya muda mrefu pamoja na matukio ya haraka yaliyochochea hali hiyo.

Akiwasilisha ripoti ya tume hiyo Aprili 23, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, amesema uchambuzi uliofanywa umeonesha kuwa zipo sababu za msingi zilizokuwa zikijengeka kwa muda mrefu, huku vichocheo vikihusisha matukio na hatua za ghafla zilizoibua ghasia hizo.

Ameeleza kuwa tume ilipokea hoja kutoka maeneo 31 yaliyotajwa na mashahidi, na baada ya uchambuzi ilibaini vyanzo vitano vikuu pamoja na vichocheo vinane vilivyochangia matukio hayo.

Miongoni mwa vyanzo vilivyotajwa ni changamoto za kisiasa zikiwemo madai ya katiba mpya, uboreshaji wa mfumo wa vyama vingi, migogoro ya ndani ya vyama pamoja na hitaji la marekebisho ya mfumo wa uchaguzi na tume huru ya uchaguzi.

Kwa upande wa uchumi, ripoti imebainisha masuala kama ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, mazingira magumu ya biashara na uwekezaji pamoja na wingi wa tozo na kodi kuwa chanzo cha malalamiko ya wananchi.

Katika eneo la kijamii, tume imeeleza kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili, kupungua kwa uzalendo na kuongezeka kwa malalamiko yanayohusisha rushwa, ubadhirifu wa mali za umma pamoja na matukio ya utekaji na kupotea kwa watu.

Jaji Chande amesema takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2003 hadi 2005, watu 758 waliripotiwa kupotea au kutekwa, ambapo 113 walipatikana, mashauri nane kufunguliwa huku watu 445 wakiwa bado hawajulikani walipo.

Ameongeza kuwa udhaifu katika utendaji wa baadhi ya watumishi wa umma, hasa ngazi za chini, pamoja na kushindwa kushughulikia kwa wakati kero za wananchi na utekelezaji hafifu wa mapendekezo ya tume zilizopita, umechangia kuongezeka kwa malalamiko.

Ripoti hiyo pia imegusia athari za uhusiano wa kimataifa, ikieleza kuwa baadhi ya mataifa hutumia mbinu mbalimbali kulinda maslahi yao katika nchi zinazoendelea, hali inayoweza kuwa na athari za kisiasa na kiuchumi.

Aidha, imebainika kuwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walitumia changamoto za wananchi kuwahamasisha kushiriki katika ghasia kupitia kaulimbiu na matamko yao.

Kuhusu vichocheo, tume imevigawa katika makundi matatu, ambapo kundi la kwanza linahusisha matumizi ya mitandao ya kijamii kuhamasisha kususia uchaguzi na kuandaa mbinu za kuzuia mchakato huo.

Kundi la pili linahusisha kaulimbiu za kisiasa zilizolenga kushinikiza mabadiliko, huku kundi la tatu likihusisha baadhi ya watu waliokatwa katika mchakato wa uteuzi ndani ya vyama, waliodaiwa kuhamasisha au kushiriki ghasia kwa maslahi ya kisiasa.

Post a Comment

0 Comments