Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amemfuta kazi Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo pamoja na Waziri wa Fedha aliyekuwa ametumikia nafasi hiyo kwa muda wa chini ya wiki mbili, vyombo vya habari vya serikali viliripoti usiku wa Jumatano.
Hatua hiyo ni sehemu ya mabadiliko ya mara kwa mara yanayoendelea kufanywa katika safu za juu za serikali ya Salva Kiir katika miaka ya hivi karibuni.
Mkuu wa Jeshi aliyefutwa kazi, Jenerali Paul Nang, alikuwa ameshika nafasi hiyo tangu Oktoba mwaka 2025, huku akikosolewa kutokana na hali ya usalama kuzidi kuzorota nchini humo. Naye Waziri wa Fedha, Salvatore Garang Mabiordit, alikuwa ameteuliwa kushika wadhifa huo Aprili 23 mwaka huu.
Wakati huo huo, Salva Kiir amemteua tena Jenerali Santino Deng Wol kuwa Mkuu mpya wa Jeshi, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la South Sudan Broadcasting Corporation. Wol anatokea eneo la Bahr El Gazal, ambako pia anatokea Rais Kiir, na aliwahi kushika nafasi hiyo kati ya mwaka 2020 hadi 2024.
Pia, Kuol Daniel Ayulo, aliyewahi kuhudumu katika Wizara ya Fedha na Wizara ya Biashara kama Katibu Mkuu Msaidizi, ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa Fedha.
Sudan Kusini inaendelea kukumbwa na changamoto katika utekelezaji wa mageuzi yaliyoainishwa kwenye makubaliano ya amani ya mwaka 2018 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano, ikiwemo kuunganisha majeshi ya nchi na maandalizi ya uchaguzi mkuu.

0 Comments