RC Chalamila Akagua Viwanja vya AFCON,Ataka Vikamilike kwa Wakati

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Viwanja vya Farasi na Leaders Club vilivyopo Wilaya ya Kinondoni, ambavyo vinatarajiwa kutumika kwa mazoezi wakati wa mashindano ya AFCON.

Katika ziara hiyo, RC Chalamila amemtaka mkandarasi kuhakikisha ujenzi wa viwanja hivyo unakamilika kwa wakati ili kuendana na maandalizi ya mashindano hayo makubwa ya Afrika.

Aidha, ameitaka Halmashauri ya Kinondoni kutumia fursa ya AFCON kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kuhamasisha utalii pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa wananchi kufanya biashara mbalimbali ili kuongeza kipato.

Akizungumza katika Viwanja vya Farasi, Chalamila amesema ni muhimu kuboresha maeneo ya fukwe ikiwemo Coco Beach ili yaweze kuvutia watalii watakaofika nchini kipindi cha AFCON. Pia amesisitiza umuhimu wa kuendeleza utalii wa vyakula vya asili vya Kitanzania kwa kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wa vyakula.

RC Chalamila pia ameweka mkazo katika kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati, akieleza kuwa hatua hiyo itakuwa sehemu ya kumpa heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake zilizowezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Akiwa Leaders Club, Mkuu huyo wa Mkoa ameelekeza kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara, huduma za maji safi na salama pamoja na mifumo ya ulinzi na usalama ikiwemo uwekaji wa taa za barabarani. Vilevile, amehimiza suala la usafi na utunzaji wa mazingira katika maeneo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, amesema maboresho ya Viwanja vya Farasi na Leaders Club hayataathiri matumizi ya kawaida ya wananchi, ikiwemo shughuli za kijamii na mbio za mwendapole ambazo zimekuwa zikisaidia wananchi kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama shinikizo la damu na kisukari.

Post a Comment

0 Comments