Rais wa Ufaransa Aanza Ziara Kenya Kwa Mkutano wa Afrika na Ufaransa

Rais wa Ufaransa ameanza ziara rasmi nchini Kenya sambamba na ufunguzi wa mkutano mkubwa wa Afrika na Ufaransa unaowakutanisha zaidi ya viongozi 30 wa Afrika pamoja na wakuu wa makampuni ya kimataifa jijini Nairobi.

Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Ufaransa na mataifa ya Afrika katika biashara, uwekezaji, teknolojia pamoja na maendeleo ya kiuchumi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ufaransa kufanya mkutano huo katika nchi inayozungumza Kiingereza tangu ulipoanzishwa miaka ya 1970.

Ziara hiyo imekuja wakati Ufaransa ikikabiliwa na changamoto ya kupungua kwa ushawishi wake katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi zilizokuwa makoloni yake ya zamani, zikiwemo Mali, Burkina Faso na Niger ambazo zimepunguza ushirikiano wake wa kijeshi na taifa hilo.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Kenya William Ruto amesema Kenya inalenga kutumia fursa hiyo kuvutia wawekezaji wa Ufaransa kupitia Soko Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) pamoja na kushinikiza mageuzi ya mfumo wa kifedha duniani ili kusaidia mataifa ya Afrika yenye changamoto ya madeni.

Ruto pia amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika elimu, teknolojia na mifumo ya kidijitali ili kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa.

“Mustakabali wetu uko kwenye teknolojia, mifumo ya kidijitali na akili mnemba,” amesema Rais Ruto.

Post a Comment

0 Comments