WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Alvaro Lario, jijini Nairobi nchini Kenya, kwa lengo la kujadili ushirikiano katika sekta ya kilimo na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Katika kikao hicho, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na IFAD katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo kinachokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya kilimo biashara, matumizi ya teknolojia ya kidijitali kwenye sekta ya kilimo pamoja na kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na IFAD katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kilimo, ukiwemo mpango wa kuongeza uzalishaji wa alizeti ili kuongeza upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.
“Kimekuwa kikao chenye mafanikio kwa sababu ushirikiano wetu na IFAD umeendelea kwa muda mrefu kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hasa katika sekta za uzalishaji,” amesema Dkt. Mwigulu.
Amesema Tanzania pia imejipanga kuendeleza mazao ya mchanganyiko ambayo hapo awali yalionekana kama mazao ya chakula pekee, lakini sasa yamekuwa sehemu muhimu ya biashara na uchumi wa nchi.
Pia Dkt. Mwigulu amesema Tanzania inatarajia kuimarisha ushirikiano na IFAD katika sekta ya mifugo pamoja na maendeleo ya mazao ya baharini Zanzibar.
“Sambamba na hayo, tunatarajia kushirikiana nao katika utekelezaji wa kilimo endelevu kinachosaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa IFAD Alvaro Lario amesema shirika hilo litaendelea kuhakikisha mipango yake inaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
“Tunatarajia kupata vipaumbele vya Tanzania ili kuona namna bora ya kusaidia katika maeneo ya usalama wa chakula, utoshelevu wa chakula pamoja na kuongeza thamani ya mazao,” amesema Lario.


0 Comments