Serikali yaimarisha mikakati ya upangaji matumizi ya ardhi vijijini.

Serikali imeeleza mikakati mbalimbali inayolenga kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi nchini, ikiwemo kuongeza kasi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi vijijini pamoja na kutumia mbinu jumuishi na shirikishi zinazowahusisha wananchi katika hatua zote za upangaji wa ardhi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jukwaa la siku tatu la wadau wa uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi mkoani Morogoro Mei 12, 2026, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, alisema serikali inalenga kupanua programu za kitaifa za upangaji ardhi vijijini kwa kushirikiana na wadau wa maeneo husika pamoja na kutumia teknolojia za kisasa na ramani za kidigitali ili kuongeza ufanisi.

Aidha, amesema serikali inakusudia kuharakisha upimaji na utoaji wa hati za kimila kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi na kuhakikisha wananchi wanakuwa na milki salama.

Mhe. Dkt. Akwilapo alisema mikakati hiyo pia inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya wizara, halmashauri, wadau na jamii katika utekelezaji wa majukumu ya sekta ya ardhi, huku serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi endelevu ya ardhi kupitia kilimo hifadhi na ufugaji unaozingatia uwezo wa ardhi.

Kwa mujibu wa waziri huyo, lengo kuu ni kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi haibaki kwenye maandalizi pekee bali inatekelezwa kwa vitendo ili kuchochea maendeleo endelevu na kupunguza migogoro katika jamii.

Ametoa rai kwa wananchi kushiriki kuchangia gharama za uandaaji wa hati za hatimilki za kimila ili kuongeza kasi ya umilikishaji wa ardhi nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema mkoa huo umeweka mikakati madhubuti ya kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kufanya tathmini ya kina na kuweka ajenda hiyo katika vikao vya kila mwezi vya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi, Joseph Mafuru, amesema kati ya vijiji 12,333 nchini, ni vijiji 4,925 pekee sawa na asilimia 39.9 vilivyo na mipango ya matumizi ya ardhi huku vijiji 7,408 vikiwa bado havijafikiwa na huduma hiyo.

Amesema changamoto kubwa zinazokwamisha kasi ya upangaji wa matumizi ya ardhi ni pamoja na uhaba wa fedha na matumizi hafifu ya teknolojia stahiki, huku akisisitiza umuhimu wa wadau kushirikiana kuweka mikakati ya pamoja ya kukamilisha zoezi hilo nchini.

Post a Comment

0 Comments