Serikali Yaimarisha Mapambano Dhidi ya Magonjwa Yasiyoambukiza Nchini

Waziri wa Afya,Omary Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za matibabu na kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kuongeza kliniki za kisukari na shinikizo la damu pamoja na kutoa elimu kwa wananchi.

Akizungumza wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027,Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha utekelezaji wa afua za kisukari, shinikizo la damu na magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji.

Amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Serikali imeanzisha kliniki mpya 130 za kisukari na shinikizo la damu na kufanya idadi ya kliniki hizo kufikia 168 kutoka kliniki 38 zilizokuwepo mwaka 2025.

Ameeleza kliniki hizo zimeboreshwa kwa kupatiwa dawa muhimu, vifaa tiba pamoja na mafunzo kwa watumishi wa afya ili kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.

Mchengerwa amesema Serikali pia imeendelea kuhamasisha wananchi kufanya uchunguzi wa afya mapema kupitia kampeni mbalimbali, ikiwemo upimaji katika maeneo ya kazi, utoaji wa elimu ya afya pamoja na matembezi ya kitaifa yanayohamasisha mazoezi.

Ameongeza kuwa Wizara ya Afya itaendelea kutumia vyombo vya habari kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ili kupunguza athari za magonjwa hayo nchini.

Post a Comment

0 Comments