Marekani yatumia dola bilioni 29 katika vita dhidi ya Iran.

Marekani imetumia takribani dola bilioni 29 katika vita dhidi ya Iran hadi sasa, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na afisa mwandamizi wa Pentagon, ikiwa ni ongezeko la dola bilioni nne kutoka makadirio yaliyotolewa mwishoni mwa mwezi uliopita.

Taarifa hiyo imekuja wakati wa mvutano wa kisiasa nchini United States kuelekea uchaguzi wa wabunge, ambapo chama cha Republican cha Rais Donald Trump kinakabiliwa na presha ya kisiasa huku Wanademokrasia wakihusisha vita hivyo na kupanda kwa gharama za maisha.

Mnamo Aprili 29, Pentagon ilikadiria gharama za vita hivyo kufikia dola bilioni 25, lakini kaimu mdhibiti wa fedha wa Pentagon, Jules Hurst, amesema gharama mpya zinahusisha ukarabati wa vifaa vya kijeshi, uingizwaji wa silaha pamoja na gharama za operesheni zinazoendelea.

Hurst alitoa taarifa hiyo mbele ya wabunge akiwa pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, na Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi, Dan Caine.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, utawala wa Trump ulikadiria kuwa siku sita za mwanzo za vita hivyo ziligharimu angalau dola bilioni 11.3.

Wakati huo huo, Israel imekadiria kuwa vita dhidi ya Iran na Lebanon kwa siku 40 viligharimu karibu dola bilioni 17.5. Katika kipindi hicho, Iran ilirusha mamia ya makombora ya balestiki kuelekea Israel na kusababisha uharibifu mkubwa pamoja na vifo vya watu.

Maafisa wa Iran wamekadiria hasara za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kufikia dola bilioni 270, kiwango kinachojumuisha uharibifu wa miundombinu na athari za kiuchumi. Iran pia imeendelea kudai fidia katika mazungumzo yake na Marekani.

Mapigano hayo yalianza baada ya Marekani kushirikiana na Israel kuishambulia Iran Februari 28, mashambulizi yaliyoripotiwa kusababisha kifo cha kiongozi wa muda mrefu wa Iran, Ali Khamenei, pamoja na viongozi wengine waandamizi na mamia ya raia.

Iran ilijibu kwa kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta duniani, huku ikiendelea kurusha makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba.

Licha ya kuwepo kwa usitishaji vita uliosimamiwa na Pakistan tangu Aprili 8, mvutano bado unaendelea huku Rais Trump akionya kuwa makubaliano hayo yako katika hali tete.

Post a Comment

0 Comments