Uturuki yaeleza matumaini ya Marekani na Iran kufikia makubaliano ya kudumu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Turkey, Hakan Fidan, amesema anaamini kuwa kwa sasa United States na Iran zinaonyesha nia ya dhati ya kusitisha vita na kufikia makubaliano ya kudumu, huku akionya kuwa kuendelea kwa mzozo huo kunaweza kuathiri uchumi wa dunia na usalama wa kikanda.

Akizungumza katika mahojiano na Al Jazeera, Fidan alisema kipaumbele cha Uturuki ni kuhakikisha usitishaji wa mapigano uliopo unaendelea kudumu ili kuzuia hali ya eneo hilo kuzorota zaidi.

Amesema kuendelea kwa vita kunaweza kusababisha maafa makubwa, kuongeza machafuko na kuathiri sekta ya nishati pamoja na uchumi wa dunia.

Fidan pia alisisitiza umuhimu wa kurejesha hali ya kawaida katika Mlango-Bahari wa Hormuz kwa kuhakikisha meli zote zinaendelea kupita kwa uhuru kama ilivyokuwa kabla ya mapigano kuanza.

Aidha, amesema Uturuki inaunga mkono juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Pakistan kwa kushirikiana na nchi nyingine za ukanda huo ikiwemo Qatar, kwa lengo la kusaidia kufikiwa kwa suluhu ya kidiplomasia kati ya Marekani na Iran.

Kwa mujibu wa Fidan, nchi za kikanda zinaendelea kushirikiana kutafuta mawazo ya kujenga yatakayosaidia kufanikisha makubaliano yatakayokubalika kwa pande zote mbili.

Post a Comment

0 Comments