Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha Uwanja wa Ndege wa Mwanza ili uweze kufikia hadhi ya kimataifa na kuendana na nafasi ya jiji hilo kama kitovu cha shughuli za kiuchumi katika Kanda ya Ziwa.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Mei 13, 2026, Nchemba alisema serikali inatambua umuhimu wa uwanja huo katika kukuza uchumi na usafiri wa anga, hivyo imeendelea kufanya maboresho yatakayowezesha kuhudumia ndege kubwa na kukidhi viwango vya kimataifa.
Alisema juhudi zinaendelea kufanyika ikiwemo mazungumzo ya kuongeza eneo la uwanja huo ili kuruhusu upanuzi wa njia ya kurukia ndege pamoja na maboresho mengine ya miundombinu.
Aidha,Waziri Mkuu huyo amesema serikali imekubaliana kujenga jengo jipya la abiria lenye hadhi ya kimataifa ambalo litakidhi mahitaji ya muda mrefu ya uwanja huo.
“Lengo ni kuwa na jengo la kisasa ambalo halitahitaji kubomolewa baada ya muda mfupi, bali litakalokidhi viwango vya viwanja vya ndege vya kimataifa,” alisema Nchemba.
0 Comments