Wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira anayeshughulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Kanizio Freddy Manyika, wamefanya kikao kazi na Shirika lisilo la kiserikali la Kazzi Africa Holdings (T) Ltd leo Mei 07, 2026 jijini Dodoma.
Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba na kuwashirikisha pia wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Lengo la kikao hicho lilikuwa kujadili utekelezaji wa programu ya “Otesha Afrika” inayolenga kuhamasisha upandaji na utunzaji wa miti katika maeneo mbalimbali nchini.
Akifungua kikao hicho,Dkt. Manyika amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha juhudi za kulinda na kuhifadhi mazingira zinakuwa endelevu.
Amesema mabadiliko ya tabianchi ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa pamoja, huku akieleza kuwa kampeni za upandaji miti zinaweza kuwa sehemu ya suluhisho na pia fursa kwa wananchi kushiriki katika uhifadhi wa mazingira.
“Sote tunatambua kuwa kila ifikapo Juni 17 tunaadhimisha Siku ya Kupambana na Kuenea kwa Jangwa, hivyo ushiriki wa wadau katika kampeni za upandaji miti unaweza kuongeza nguvu katika mapambano hayo,” amesema Dkt. Manyika.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Kazzi Africa Holdings (T) Ltd, Bw. Rumisho Shikonyi, amesema kuna umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau ili kuhakikisha utamaduni wa kupanda na kutunza miti unaendelea kuimarika nchini.
Aidha, washiriki wa kikao hicho walisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya upandaji miti kwa watoto na vijana, pamoja na kuimarisha mfumo wa usimamizi, ufuatiliaji na utunzaji wa takwimu za miti inayopandwa nchini.



0 Comments