Tanzania imekamilisha maandalizi ya Mfumo wa Taifa wa Kurejesha Hali Baada ya Maafa, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa nchi katika kukabiliana na athari za majanga na kurejesha haraka huduma muhimu kwa wananchi na shughuli za kiuchumi.
Mfumo huo ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kukabiliana na ongezeko la maafa yanayochangiwa na mabadiliko ya tabianchi, ukiweka mkazo katika matumizi ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya tathmini ya haraka ya madhara na hasara zinazotokana na majanga.
Akizungumza katika Mkutano wa Sita wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa wa nchi za SADC uliofanyika Masvingo nchini Zimbabwe, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, aliyemwakilisha Prof. Palamagamba Kabudi, alisema mfumo huo utawezesha tathmini sahihi ya uharibifu katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, uzalishaji wa kiuchumi na huduma za kijamii.
Alisema pia mfumo huo umeweka utaratibu wa kuwa na mipango jumuishi ya kurejesha hali katika maeneo yaliyoathirika huku ukisisitiza kuingizwa kwa masuala ya maafa katika mipango na bajeti za maendeleo za taifa na serikali za mitaa.
Katika hatua nyingine, Tanzania imezindua Mwongozo wa Taifa wa Ugharamiaji wa Maafa wa mwaka 2025 wenye lengo la kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa maafa na kurejesha hali kupitia vyanzo vya ndani na nje ya nchi.
Mhe. Mmuya alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya serikali kuimarisha mifumo ya kisera na ushirikiano wa kikanda, kimataifa pamoja na sekta binafsi katika kukabiliana na maafa.
Aidha, alisema Tanzania inaendelea kuwekeza katika mifumo himilivu ya chakula na kilimo kupitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT), kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia, taarifa za hali ya hewa na ujenzi wa miundombinu inayozingatia vihatarishi vya majanga.
Tanzania pia imezialika nchi wanachama wa SADC kutembelea nchini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika matumizi ya teknolojia za usimamizi wa maafa, mifumo ya tahadhari ya mapema pamoja na maendeleo ya Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa kinachotarajiwa kuwa kituo cha umahiri katika ukanda huo.


0 Comments