TRA Tanga Yatoa Elimu ya Kodi kwa Wanawake Wafanyabiashara na Wajasiriamali

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imeendelea kutoa elimu ya mlipakodi pamoja na kuainisha fursa mbalimbali kwa wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali zaidi ya Mia Tatu(300)wote kutoka mkoa wa Tanga.

Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanawake kuelewa vyema mifumo na sheria za kodi nchini ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza katika kongamano la Wanawake na Kodi lililofanyika mkoani Tanga, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, amesema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika ulipaji wa kodi nchini.

Amesema kwa sasa wanawake wengi wameendelea kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa wajibu huo muhimu wa maendeleo ya Taifa.

“TRA inatambua mchango wa wanawake katika ulipaji wa kodi, na kwa sasa wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kulipa kodi nchini,” alisema Castro.

“Hivyo niwaombe muendelee kushiriki kikamilifu katika kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa letu,” aliongeza.

Aidha, Castro aliwahimiza wanawake hao kuendelea kudumisha nidhamu ya ulipaji wa kodi huku akisisitiza kuwa TRA ipo tayari kutoa msaada kwa wafanyabiashara wanaokutana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na kodi.

“TRA ipo tayari kuwasaidia wafanyabiashara wote wanaopitia changamoto mbalimbali, hivyo mnapokutana na tatizo lolote msisite kufika TRA kupata msaada,” alisisitiza Castro.

Post a Comment

0 Comments