Na Mwandishi Wetu, kata ya Bwembwera.
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA amesema endapo atachaguliwa ataongeza nguvu katika utatuzi wa migogoro ya ardhi katika kata ya Bwembwera ili kuwawezesha wananchi watumie ardhi hiyo kiuchumi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Bwembwera, MwanaFA alisema kuwa uwepo wa migogoro ya ardhi umekuwa ukimkosesha usingizi kwakuwa wananchi wanashindwa kutumia ardhi kwa shughuli zao za kilimo.
"Ndugu zangu endapo mtanichagua katika miaka mitano ijayo tutahakikisha tunaongeza nguvu katika utatuzi wa migogoro ya ardhi," alisema.
MwanaFA alitolea mfano mgogoro wa shamba la mkonge Bwembwera Estate ambalo linahusisha kata nne za Makole, Mbwembwera, Kwafungo na Potwe. Mgogoro wa shamba hilo upo Mahakamani.
Mgombea huyo aliwasihi wananchi wa kata hiyo kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura kuchagua viongozi wa CCM ili waweze kupata haki ya kudai maendeleo katika maeneo yao.
"Hakuna haki inayokuja bila wajibu ndugu zangu, Kila mmoja aende akapige kura ni wajibu wenu wa kikatiba," alisema na kuongeza,
"Kamchagueni Rais Samia Suluhu Hassan, nichagueni Mimi kijana wenu lakini pia mchagueni diwani wenu Ali Nyangasa,".
Alisema maana halisi ya kupiga kura ni hatua ya maendeleo katika kitongoji, kijiji na kamwe wasiwe na mtizamo hasi kwamba CCM itashinda tu katika uchaguzi huo bila kupiga kura.
"Ndugu zangu ni kweli CCM itashinda lakini CCM isingependa ishinde bila kura yako, nendeni mkawachague wagombea wa CCM Oktoba 29," alisema.
MwanaFA CCM inazo sababu kwanini wanatakiwa kuichagua ni sababu imetekeleza kwa kiasi kikubwa ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa kuleta miradi mingi kwenye kata hiyo ambapo ilipata jumla ya shilingi bilioni 1.6.
Akitoa mchanganua wa fedha hizo katika miradi mbalimbali, MwanaFA alisema shilingi milioni 64.4 zililetwa kwa ajili ya ujenzi wa darasa, umaliziaji wa maabara na matundu ya vyoo katika shule ya sekondari Bwembwera.
Katika elimu ya msingi zilipelekwa shilingi milioni 247.5 kwa ajili ya shule za Mamboleo, Msowero, Mianga na Bwembera kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, vyoo na ununuzi wa vifaa vya tehama.
Kwa upande wa maji walipata mradi wa maji Mizembwe ambao uligharimu shilingi bilioni 1.4 na hadi utakapokamilika utahudumia vitongoji 18 kati ya 20 vya kata hiyo.
Kwa upande wa mfuko wa Jimbo alipeleka saruji tani 4 shule ya msingi Msowero, bati 20 shule ya Mkului na shilingi milioni 1 ya ujenzi wa tenki na gata la kuvuna maji ya mvua katika shule ya msingi Bwembwera.
Fedha nyingine alitoa shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya umaliziaji wa ofisi ya mtendaji Kijiji cha Msowero, shilingi 500 ujenzi wa darasa shikizi Muskat na wanawake wa UWT walipewa shilingi laki Tano kwa ajili ya mradi wao wa viti.
Kwa upande wa mikopo katika kata hiyo kikundi cha vijana kilipata shilingi milioni 14.8 lakini pia alitoa rai kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wajitokeze kuomba mikopo ambayo inatolewa na halmashauri.
0 Comments