DKT.MIGIRO:SIASA YA CCM NI YA KUWAJENGA NA KUWASHAWISHI WANANCHI KWA HOJA

Makamu wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Dkt. Asha-Rose Migiro, amesema siasa ya CCM inalenga kuwajenga wananchi na kuwashawishi kwa hoja zenye maslahi kwa Taifa, jambo linalokifanya chama hicho kuendelea kuwa juu kuliko vyama vingine vya siasa nchini.

Dkt. Migiro ameyasema hayo leo mapema alipokuwa akizungumza na Mabalozi wa Mashina katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, ambapo ameeleza kuwa CCM imejijengea msingi imara wa siasa zinazozingatia mahitaji ya wananchi na kushughulikia changamoto zao kwa hoja na vitendo.

Amesisitiza kuwa CCM ina jukumu kubwa la kuimarisha utaratibu wa kukutana mara kwa mara kupitia vikao vya mashina, pamoja na kudumisha mahusiano ya karibu ya kila siku kati ya wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla, wakiwemo wasiokuwa wanachama wa chama hicho.

Aidha, Dkt. Migiro amesema itikadi ya CCM itaendelea kuthamini utu wa mwanadamu na kujengwa katika misingi ya ujamaa na kujitegemea, kama ilivyoasisiwa na waasisi wa chama hicho, kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kitaifa na maendeleo endelevu.

Ameongeza kuwa kauli mbiu ya CCM inayosema “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele” inaendelea kuwa dira ya chama hicho katika kuwatumikia wananchi, akisisitiza kuwa maendeleo ya Taifa hayawezi kupatikana bila kuthamini utu na kufanya kazi kwa bidii.

Post a Comment

0 Comments