Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekutana na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yoichi Mikami, na kujadili masuala ya uchumi, utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na uwekezaji.
Akizungumza na Balozi huyo leo Jumatano, Januari 14, 2026, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Dkt. Mwigulu ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara ya Arusha–Holili, Bandari ya Kigoma, miradi ya kilimo pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba kwa huduma za afya ya mama na mtoto.
Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kukamilishwa kwa wakati kama ilivyopangwa.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutuma salamu za pongezi kwa Waziri Mkuu wa Japan, Bi. Sanae Takaichi, kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo tangu Oktoba 2025, hatua iliyoweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo nchini Japan. Amesema Tanzania inaendelea kuthamini na kuimarisha ushirikiano wa karibu na Japan kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa upande wake, Balozi Mikami amemueleza Waziri Mkuu kuwa ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya kijamii 79 ambayo awali ilikuwa inasuasua, ambapo kuanzia Septemba 2024 hadi sasa imebakia miradi 16 pekee.
Amesema Japan itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania, ushirikiano ambao umeendelea kwa zaidi ya miaka 60.
.jpeg)
.jpeg)

0 Comments