Kreta ya Empakaai ni mojawapo ya kreta za volkano zilizopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, ikiwa na kingo za juu na ziwa zuri linalofunika zaidi ya asilimia 75 ya sakafu ya kreta. Kivutio kikubwa ndani ya kreta hii ni uwepo wa idadi kubwa ya ndege aina ya heroe (flamingo) wanaoonekana kando ya ufukwe wa ziwa, ambapo wanapokusanyika kwa wingi hulifanya ziwa lionekane lenye rangi ya waridi (pinki).
Kreta hii iliyopo katika nyanda za juu za Ngorongoro imezungukwa na kuta za misitu yenye mteremko mkali wa takribani mita 300 kwa urefu, zikiwa na uoto wa asili wa kijani kibichi pamoja na makazi ya wanyamapori na aina mbalimbali za ndege. Eneo la kreta lina upana wa takribani kilomita 8, huku karibu nusu ya sakafu yake ikifunikwa na ziwa lenye magadi na kina kirefu, ambalo ni makazi ya heroe (flamingo) na ndege wengine wa majini.
Kutoka juu ya ukingo wa Kreta ya Empakaai, wageni wanaweza kushuhudia mandhari ya kuvutia ya Mlima Oldoinyo Lengai, Bonde la Ufa (Great Rift Valley) pamoja na Ziwa Natron. Aidha, wageni wanaweza kufurahia matembezi ya asili kuanzia juu ya kreta au kushuka hadi sakafuni ili kushuhudia kwa karibu vivutio vilivyopo.
Empakaai ina kimo cha takribani mita 3,200 kutoka juu ya usawa wa bahari upande wa magharibi na mita 2,590 upande wa mashariki. Kutokana na mwinuko wake, eneo hili mara nyingi hufunikwa na ukungu, hali inayolifanya ziwa lionekane na rangi ya kijani kibichi au buluu ya kina.
Kreta ya Empakaai ni maarufu kwa safari za kutembea kwa miguu, ambapo watalii hutembea kwa takribani saa mbili na nusu kwenda na kurudi, kulingana na uwezo wa mwili. Katika matembezi hayo, wageni hupata fursa ya kuona kwa ukaribu ziwa, msitu mnene pamoja na mazingira ya asili yanayozunguka sakafu ya kreta.
Kivutio hiki kinaweza kutembelewa wakati wowote wa mwaka, ingawa kipindi kinachopendekezwa zaidi ni kuanzia mwezi Juni hadi Desemba, ambacho ni msimu wa kiangazi.



0 Comments