Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ndugu Fadhili Maganya, ametoa maagizo kwa viongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na Afisa Elimu Sekondari kuhakikisha wanawasiliana naye mara moja kwa njia yoyote, kufuatia kushindwa kwao kufika katika eneo la tukio licha ya kupata taarifa za ujio wake katika shule hiyo.
Maganya ametoa maagizo hayo leo Januari 14, 2026, alipotembelea Shule ya Sekondari Hombolo iliyopo Kata ya Hombolo Bwawani, ambapo alizungumza na wanafunzi wa shule hiyo na kukabidhi misaada mbalimbali ya vifaa vya shule kwa niaba ya wanafunzi nchini kote.
Akizungumza katika tukio hilo, Mwenyekiti huyo amesema hali ya viongozi husika kushindwa kufika shuleni hapo wakati yeye amefika kwa ajili ya kushughulikia masuala ya shule haiwezi kuvumiliwa, akisisitiza uwajibikaji kwa viongozi wote wa ngazi husika.
“Siwezi kufika shuleni kushughulikia masuala ya maendeleo ya shule halafu viongozi wanaohusika hawapo. Jambo hili haliwezi kuvumilika. Nawataka waje haraka na ndani ya wiki mbili nataka kuona Mwenyekiti wa Bodi na Mkuu wa Shule tayari mmepata hati ya umiliki wa eneo la shule,” amesema Maganya.
Ameeleza kuwa shule nyingi hukosa hati za umiliki wa ardhi, hali inayosababisha migogoro ya mipaka, ambapo wananchi huanza kuchukua maeneo ya shule hatua kwa hatua na kusababisha migogoro ya mara kwa mara.

0 Comments