Na.Mwandishi Wetu – Nkasi
Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu imewajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, kwa lengo la kuhakikisha jamii inakuwa stahimilivu wakati wa majanga na maafa.
Elimu hiyo imetolewa leo, Januari 19, 2026, na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati wa kikao cha kupitia rasimu za nyaraka za usimamizi wa maafa za Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Kikao hicho kiliwahusisha Kamati za Usimamizi wa Maafa wilayani humo na kuongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.
Kikao hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na timu ya wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, kikilenga kuwapitisha wajumbe katika nyaraka zilizoandaliwa kwa ajili ya matumizi ya Halmashauri.
Nyaraka hizo ni pamoja na Tathmini ya Vihatarishi vya Majanga, Tathmini ya Uwezekano wa Kuathirika na Uwezo wa Kukabiliana na Majanga, Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa, pamoja na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa.
Akitoa neno la shukrani mara baada ya kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Bw. Eliud Njogellah, amepongeza kazi iliyofanywa na timu ya waandaaji wa nyaraka hizo.
Ameeleza kuwa nyaraka hizo zimekuja kwa wakati muafaka, hasa ikizingatiwa kuwa Halmashauri imekuwa ikikumbwa na majanga na maafa mbalimbali, hivyo zitatumika kwa uzito unaostahili ili kuleta tija iliyokusudiwa katika kulinda maisha na mali za wananchi.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
0 Comments