Raia wawili wa Uturuki pamoja na dereva wao ambaye ni raia wa Ethiopia wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wenye silaha, walipokuwa katika safari ya utalii nchini Ethiopia.
Taarifa hiyo imetolewa na Balozi wa Uturuki nchini Ethiopia, Berk Baran, ambaye aliliambia Shirika la Habari la Anadolu kuwa shambulio hilo lilitokea asubuhi ya Januari 12 katika eneo la vijijini karibu na mji wa Tum, kusini-magharibi mwa Ethiopia.
Waathirika waliotambuliwa kuwa ni raia wa Uturuki ni Erdogan Akbulak na Cengizhan Gungor, pamoja na dereva wao ambaye ni raia wa Ethiopia, amesema balozi huyo.
Kwa mujibu wa Balozi Baran, raia wanne wa Uturuki walikuwa wakisafiri kwa magari mawili tofauti wakati wa shambulio hilo. Alisema watu wawili waliokuwa kwenye gari lililokuwa mbele waliweza kutoroka bila kujeruhiwa na baadaye walitoa taarifa kwa ubalozi wa Uturuki kuhusu tukio hilo.
Ameongeza kuwa raia wa Uturuki walionusurika pamoja na miili ya waliouawa ilisafirishwa kwa ndege hadi Addis Ababa asubuhi ya Jumanne.
“Taratibu zote zinaendelea. Raia wetu walionusurika wanahifadhiwa katika ubalozi, huku miili ya marehemu ikitarajiwa kusafirishwa kwenda Istanbul kwa ndege ya Turkish Airlines leo usiku, ikitarajiwa kuwasili kesho asubuhi,” amesema Balozi Baran.

0 Comments