Rais Samia: Mahakama Huru ni Nguzo ya Utawala Bora na Maendeleo ya Taifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kulindwa kwa uhuru wa Mahakama na wajibu wa majaji na mahakimu katika kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi wote. Amesema Mahakama huru ndiyo nguzo muhimu ya utawala bora, amani na maendeleo endelevu ya Taifa.

Rais Samia ametoa kauli hiyo Januari 13, 2026, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofanyika katika Makao Makuu ya Mahakama, jijini Dodoma. Amebainisha kuwa majukumu ya majaji na mahakimu ni mazito na yanahitaji weledi, uadilifu, uvumilivu, busara na ujasiri wa kusimamia haki bila woga, upendeleo wala rushwa.

Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mhimili wa Mahakama, ikiwemo kuboresha miundombinu, kuongeza rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuharakisha utoaji wa haki.

Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Mahakama ina nafasi muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025–2050, hasa katika kusimamia migogoro ya kibiashara, kodi na mikataba ya uwekezaji inayohusisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, kwa lengo la kulinda haki za wananchi na maslahi ya Taifa.

Kuhusu maslahi ya majaji na mahakimu, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuboresha mishahara na mazingira ya kazi kadri hali ya uchumi wa nchi itakavyoruhusu. Ameongeza kuwa changamoto zilizowasilishwa, ikiwemo migogoro ya ardhi na mapendekezo ya mabadiliko ya sheria, zimepokelewa na Serikali na zitafanyiwa kazi kadri rasilimali zitakavyopatikana.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Mcheche Masaju, amesema ushiriki wa Rais Samia katika mkutano huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uhuru wa Mahakama na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki. Ameeleza kuwa maboresho ya majengo, vitendea kazi, rasilimali watu na TEHAMA yataongeza kasi na ufanisi wa utoaji wa haki nchini.

Mkutano Mkuu wa TMJA 2026 umewakutanisha majaji na mahakimu kutoka ngazi zote nchini, ukilenga kujadili masuala ya kitaaluma, kimaadili na kiutumishi kwa lengo la kuimarisha mhimili wa Mahakama na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments