Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Januari 17, 2026 ameongoza kikao cha kazi kilichojadili ujenzi wa miradi ya barabara za haraka (Express Ways) kwa mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP). Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wakuu wa Serikali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega pamoja na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile.
Viongozi wengine walioshiriki ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. James Kilabuko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara pamoja na watendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC).
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa miradi ya barabara za haraka katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kurahisisha usafirishaji na kupunguza gharama za usafiri, huku akielekeza maandalizi ya miradi hiyo yazingatie uwazi, tija na maslahi mapana ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, Bw. David Kafulila, amesema kituo hicho kitaendelea kushirikiana na wizara husika pamoja na sekta binafsi ili kuhakikisha miradi ya barabara za haraka inatekelezwa kwa ufanisi kupitia mfumo wa PPP.



0 Comments