Wanajeshi wameanza kuonekana katika mitaa ya mji wa Johannesburg, mji mkubwa zaidi nchini Afrika Kusini, kufuatia hatua ya serikali kuagiza jeshi kusaidia polisi kukabiliana na vurugu za magenge ya uhalifu na uchimbaji haramu wa madini.
Hatua hiyo inafuatia tangazo lililotolewa mwezi uliopita na Rais Cyril Ramaphosa, aliyesema serikali itaongeza nguvu ya usalama kwa kupeleka wanajeshi kusaidiana na polisi katika kudhibiti uhalifu unaoongezeka katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Wanajeshi hao wameanza doria katika maeneo kadhaa ya Johannesburg, hususan eneo la Riverlea, ambalo limekuwa likikumbwa na matukio ya uhalifu yanayohusishwa na magenge pamoja na uchimbaji haramu wa madini.
Katika hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa, Rais Ramaphosa alisema magenge ya wahalifu yamekuwa tishio kubwa kwa demokrasia ya Afrika Kusini pamoja na maendeleo ya kiuchumi ya nchi.
Hata hivyo, Polisi wa Afrika Kusini na Wizara ya Ulinzi ya Afrika Kusini, ambayo inasimamia jeshi, hawakutoa maelezo ya kina kuhusu operesheni hiyo ya kijeshi.
Kwa mujibu wa takwimu za usalama, Afrika Kusini ina kiwango kikubwa cha mauaji ambapo wastani wa watu karibu 60 huuawa kila siku. Baadhi ya matukio hayo yanahusishwa na mapigano kati ya magenge ya dawa za kulevya katika maeneo ya Cape Town, pamoja na mashambulizi ya silaha yanayohusiana na uchimbaji haramu wa madini katika mkoa wa Gauteng.
Serikali inaamini hatua ya kupeleka wanajeshi kusaidia polisi itasaidia kupunguza uhalifu na kurejesha usalama katika maeneo yaliyoathirika.

0 Comments