Umoja wa Mataifa Wapongeza Hatua za Serikali Kufuatia Matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025


                                     

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 11 Machi 2026 amepokea salamu maalum kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, zilizowasilishwa na Mjumbe wake Maalum, Parfait Onanga-Anyanga, katika Ikulu ya Chamwino.

Bw. Onanga-Anyanga yuko nchini Tanzania kwa ziara maalum ya kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali na kutathmini hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na kuendeleza misingi ya utawala wa sheria kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoripotiwa kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza baada ya kukutana na Rais Samia, Bw. Onanga-Anyanga amesema Umoja wa Mataifa unatambua na kupongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kufuatia matukio hayo, ikiwemo uamuzi wa kuunda Tume Huru ya Uchunguzi pamoja na dhamira ya kufanya mazungumzo jumuishi ya kitaifa na kuendeleza mchakato wa mabadiliko ya Katiba.

Amesema Tanzania inaendelea kutambulika kimataifa kama nchi yenye historia ya kudumisha amani, utulivu wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa, huku pia ikitambuliwa kwa mchango wake katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani barani Afrika.

Katika ziara yake nchini, Bw. Onanga-Anyanga amekutana na viongozi wa taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahakama ya Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.

Aidha, amefanya mazungumzo na Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa Tume Huru ya Uchunguzi na wadau wengine wa kisiasa na kijamii ili kupata maoni na mitazamo tofauti kuhusu matukio yaliyotokea na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali.

Kwa mujibu wa Bw. Onanga-Anyanga, mashauriano hayo yatauwezesha Umoja wa Mataifa kupata taswira halisi ya matukio ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kutatua changamoto zilizojitokeza wakati na baada ya uchaguzi huo.

Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shukrani kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kutuma ujumbe maalum nchini Tanzania ili kupata uelewa wa kina kuhusu hali ya nchi na kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali.

Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio hayo unafanyika kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, uwajibikaji na haki, huku ikiendelea kulinda amani, umoja wa kitaifa na utulivu wa kisiasa ambao ni msingi muhimu wa maendeleo ya nchi.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali iko tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayowasilishwa na Tume Huru ya Uchunguzi mara baada ya kukamilika kwa kazi yake, akisisitiza kuwa mapendekezo hayo yatakuwa sehemu muhimu ya kuimarisha maridhiano ya kitaifa na kuendeleza mchakato wa marekebisho ya Katiba.

Rais Samia pia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa pamoja na jumuiya nyingine za kimataifa katika kukuza demokrasia, utawala bora na maendeleo jumuishi kwa manufaa ya wananchi.

Post a Comment

0 Comments