Serikali imesema itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB) ili kuhakikisha sekta ya uhandisi na teknolojia inachangia kikamilifu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 7, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, aliyemwakilisha Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 8 wa Mafundi Sanifu Tanzania wa mwaka 2026.
Akizungumza katika mkutano huo, Msando amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa mafundi sanifu na wataalamu wa uhandisi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja, reli, majengo na miundombinu mingine muhimu.
Amesema ili kufikia malengo ya maendeleo ya teknolojia na uchumi wa kisasa, ni muhimu kwa ERB kuendelea kusajili mafundi sanifu wenye sifa na weledi watakaoongeza nguvu kazi ya kitaalamu inayohitajika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi na viwango vinavyokubalika.
“Serikali itaendelea kushirikiana na ERB kuhakikisha taaluma ya uhandisi inaendelea kuimarika, huku wataalamu wakizingatia maadili, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa,” amesema Msando.
Aidha, amewataka wahandisi na mafundi sanifu wapya waliokula kiapo katika mkutano huo kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na weledi mkubwa ili miradi inayotekelezwa iwe na tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi ERB, Profesa Bakari Mwinyiwiwa, amesema bodi hiyo itaendelea kuweka mazingira bora ya kukuza taaluma ya uhandisi nchini pamoja na kuimarisha usimamizi wa wataalamu ili kuhakikisha huduma za uhandisi zinakuwa salama, bora na zinazoendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani.
Mkutano huo wa siku mbili umewakutanisha mafundi sanifu, wahandisi, wadau wa sekta ya ujenzi pamoja na wanafunzi wa taaluma za uhandisi kutoka taasisi mbalimbali za elimu, kwa lengo la kujadili nafasi ya teknolojia, ubunifu na utaalamu katika kuharakisha maendeleo ya Tanzania kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.





0 Comments