Tshisekedi Afungua Mlango wa Muhula wa Tatu DRC

Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema yuko tayari kugombea urais kwa muhula wa tatu iwapo wananchi wa nchi hiyo watamuunga mkono kupitia kura ya maoni.

Tshisekedi mwenye umri wa miaka 62 alitoa kauli hiyo Jumatano wakati akizungumza na waandishi wa habari, akieleza kuwa kwa sasa hana mpango wa kuongeza muda wa uongozi wake zaidi ya mihula miwili inayoruhusiwa na Katiba ya nchi hiyo, ambayo inatarajiwa kumalizika mwaka 2028.

“Sijawahi kufikiria kuwania muhula wa tatu, lakini kama wananchi wa Kongo watataka niendelee kuiongoza nchi yao, nitakubali,” amesema Tshisekedi.

Aidha, amesema mabadiliko yoyote ya Katiba yatakayoruhusu hatua hiyo yatafanyika kwa kuzingatia matakwa ya wananchi kupitia kura ya maoni.

Wakati huohuo, Tshisekedi ameonya kuwa hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaweza kuathiri uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwaka 2028.

Mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda yameendelea kuongezeka katika majimbo yenye utajiri wa madini ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Post a Comment

0 Comments