Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoa wa Tanga,Salum Masinde
************
Wakala wa Vipimo nchini mkoa wa Tanga,wamefanya ukaguzi na kuwakamata wafanyabiashara wa gesi kumi na tisa(19)katika wilaya za Tanga na Muheza kwa kosa la kutokuwa na mizani za kupimia gesi,pamoja na Nembo ya kuonyesha gesi inaujazo kiasi gani,kwa ajili ya kumuhakikishia mteja usahihi wa bidhaa anayonunua.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoani hapa Salum Masinde alipokua akitoa taarifa hiyo ofisini kwake amesema baada ya kupata malalamiko kwa baadhi ya wateja ambao walidai kupunjwa gesi za kwenye mitungi ndipo walipoamua kufanya ukaguzi ili kujiridhisha.
Masinde amesema katika wilaya ya Tanga waliwakamata wafanyabiashara kumi na Wilaya ya Muheza waliwakamata wafanyabiasara tisa ambao wote kwa pamoja walifikishwa katika ofisi za vipimo.
"Tulipofanya ukaguzi tumegundua wafanyabiashara wenye makosa mbalimbali, lakini kubwa ni kutokuwa na mizani za kupimia gesi ili kumuhakikishia mteja kwamba gesi anayonunua ni sahihi, kwa mujibu wa sheria ya vipimo kutokuwa na mizani kosa, lakini kosa jingine mitungi waliyonayo haikuwa na nembo yoyote kuonyesha ina uzito gani au ujazo gani kama sheria inavyotaka" alisema Masinde.
Masinde amebainisha kuwa ukaguzi huo walifanya kuanzia kwa wauzaji wa rejareja na jumla pamoja na wajazaji,lakini walipofika kwa wajazaji walikuta wanajaza vizuri na hata kwa wauzaji nao wako vizuri lakini tatizo lao hawana mizani za kuhakiki.
"Kwa maana hiyo sasa hatua tulizochukua baada ya kuwakuta na makosa hayo ya kutokuwa na mizani tuliwaleta ofisini kwetu pamoja na baadhi ya ile mitungi yao iliyokutwa na makosa,tuliwapa elimu juu ya nini sheria inataka, lakini pia tuliwaamrisha kila mmoja mpaka kufikia tarehe 28 mwezi huu wa sita wawe tayari wameshaweka mizani na kuja kuripoti na kuchukua vielelezo vyao ambavyo ni mitungi yao" alisema Masinde.
Aidha Masinde alibainisha kwamba kuanzia mei 11 walifanya ukaguzi wa kushtukiza katika vituo vya mafuta vilivyopo jijini Tanga baada ya kupata malalamiko kwa wananchi lakini walikuta vituo vyote walivyotembelea hawakukuta makosa yaliyolalamikiwa ya upunjaji wa mafuta.
"Tulifanya ukaguzi huo na mashine zote zile za kusukumia mafuta ambazo zina kasoro ndogo ndogo anbazo siyo za kiufundi zimerekebishwa, kwahiyo hadi kufikia juni 20 mashine zote zilikuwa sawa, hivyo niwatoe hofu wananchi kwamba waendelee kutumia kituo chochote cha mafuta kwakuwa mashine zote zinapima vizuri" alisema Masinde.
"Lakini hatuishii hapo, hata kama tumepima na ziko vizuri, ofisi hii ya Wakala wa Vipimo bado inaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza pale ambapo inaona inafaa,na nitoe wito kwa wananchi wote pia wanapoona kuna mashaka kuhusu vipimo au kwenye vituo vya mafuta, waje hapa ofisini kutoa taarifa na sisi tutachukua hatua ya kwenda kukagua mara moja" alisema Masinde.

0 Comments