Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Partobass Katambi (Mb), amesema Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) lina nafasi muhimu katika kulinda ushindani wa uchumi wa Taifa katika mazingira ya uchumi wa dunia unaotawaliwa na sayansi, teknolojia na maarifa.
Akizungumza leo Desemba 22, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kikao na Menejimenti ya TIRDO, Mhe. Katambi amesema ushindani wa kiuchumi wa sasa unategemea ubunifu, uvumbuzi na tafiti za kisayansi, hali inayozilazimu nchi kuimarisha uwekezaji katika taasisi za utafiti ili kufikia maendeleo endelevu.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya viwanda hayawezi kupatikana bila sera imara zinazojengwa juu ya ushahidi wa kisayansi, akibainisha kuwa tafiti zinazofanywa na taasisi za kitaifa kama TIRDO ndizo msingi wa maamuzi sahihi ya kisera na uwekezaji wa kimkakati.
Naibu Waziri huyo ameipongeza TIRDO kwa kuendelea kuimarisha rasilimali watu kupitia uwepo wa watafiti waliobobea, wakiwemo wenye shahada za uzamivu na maprofesa, pamoja na programu za kujengea uwezo wa kitaalamu, hatua inayoiwezesha taasisi hiyo kutoa ushauri wa kitaalamu unaokubalika ndani na nje ya nchi.
Aidha, amepongeza mchango wa TIRDO katika tafiti za uhifadhi wa chakula, maendeleo ya teknolojia za uzalishaji wa viwandani na kukuza ubunifu wa ndani unaochochea ajira, kuongeza thamani ya bidhaa na kupanua masoko ya Tanzania.
Mhe. Katambi amesisitiza umuhimu wa kuelekeza tafiti katika kubaini fursa za kufufua au kubadili matumizi ya viwanda vilivyokwama ili viendelee kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Akihitimisha ziara yake, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika maboresho na ujenzi wa majengo ya TIRDO yaliyoanzishwa tangu mwaka 1984, akisema hatua hiyo imeimarisha mazingira ya kazi na uwezo wa taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake.



0 Comments