Kibaha, Pwani
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), imeendesha mafunzo ya siku nne kwa watumishi wapya 20 walioajiriwa katika ofisi hiyo, yakilenga kuwajengea uwezo wa kiutendaji na kuimarisha ufanisi katika utumishi wa umma.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, kuanzia Januari 13 hadi 16, 2026.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Chacha Marigiri, kwa kushirikiana na wakufunzi kutoka TPSC, wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja pamoja na wataalamu wa fedha na uwekezaji kutoka Mfuko wa Uwekezaji wa UTT AMIS.
Akitoa mada kuhusu matumizi sahihi ya muda, Bw. Marigiri alisisitiza umuhimu wa kupanga vipaumbele na kuweka uwiano kati ya kazi na maisha binafsi ili kuongeza ufanisi kazini na kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri utendaji wa mtumishi wa umma.
“Watumishi wengi hushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na matumizi duni ya muda na kukosa mpangilio wa vipaumbele,” alisema.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa TPSC, Mhadhiri wa chuo hicho, Bw. Hosea George, alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa watumishi wapya kwani yanawajengea misingi ya utendaji kazi kwa kuzingatia maadili, sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuchochea maendeleo ya Serikali, pamoja na taasisi na mashirika ya umma yanayosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mada zilizofundishwa ni pamoja na maadili na utendaji katika utumishi wa umma, muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uendeshaji wa shughuli zake Tanzania Bara na Zanzibar, mapitio ya sheria za utumishi wa umma, elimu ya afya ikiwemo UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili, upimaji wa utendaji kazi wa watumishi, pamoja na elimu ya fedha na utamaduni wa kuweka akiba.
Akitoa mada ya afya, Dkt. Frank Mlaguzi kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam aliwataka watumishi wa umma kuzingatia utunzaji wa afya zao kwa kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na homa ya ini, pamoja na changamoto za afya ya akili, akibainisha kuwa magonjwa hayo huathiri kwa kiasi kikubwa ufanisi kazini.
Mwisho wa mafunzo hayo, Bw. Chacha Marigiri aliwatunuku vyeti wahitimu na kukipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kuendesha mafunzo yenye tija, akieleza kuwa yamewajenga watumishi wenye maadili, nidhamu, bidii na weledi.
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Goodluck Mtebene, mtumishi mpya katika Kurugenzi ya Fedha na Uhasibu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, aliishukuru OMH na TPSC kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema yamekuwa mwongozo muhimu katika kuuelewa vyema utumishi wa umma na utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia maadili waliyojifunza.



0 Comments