TANGA YAANZA MWAKA 2026 KWA KUWA MWENYEJI WA WIKI YA HUDUMA ZA FEDHA KITAIFA

Ikiwa ni takribani siku 19 tangu kuanza kwa Mwaka Mpya wa 2026, Mkoa wa Tanga, unaotambulika kwa utulivu na jamii yenye ustaarabu wa amani, umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa.

Maadhimisho hayo, yanayoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Fedha, wadau wa sekta ya fedha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, yatafanyika kuanzia Januari 19 hadi 26, 2026, katika Uwanja wa Usagara jijini Tanga.

Mamia ya washiriki kutoka taasisi mbalimbali tayari wamewasili jijini Tanga na kuanza kushiriki hatua za mwisho za maandalizi ya maadhimisho hayo, ikiwemo kuandaa na kuweka huduma zao katika mabanda yaliyotapakaa ndani ya uwanja huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, amesema maadhimisho hayo yenye kauli mbiu “Elimu ya fedha, msingi wa maendeleo ya kiuchumi” yatafunguliwa rasmi na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar.

Ameeleza kuwa maadhimisho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020 hadi 2030, unaolenga kuweka vipaumbele katika utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa umma pamoja na kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Stella Anastazi, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi, hususan katika masuala ya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji.

Naye Meneja Mahusiano na Uhamasishaji wa Mfuko wa SELF Microfinance Ltd, Bi. Linda Mshana, amesema taasisi hiyo itatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya fedha, hususan kwa wananchi wanaonufaika na huduma za mikopo.

Awali, Bi. Mjema amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa FinScope wa mwaka 2023, ni asilimia 53.5 pekee ya nguvu kazi nchini iliyokuwa ikitumia huduma rasmi za fedha.

Ameongeza kuwa hali hiyo inaacha kundi kubwa la Watanzania bila kunufaika na huduma hizo, jambo linalowanyima fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli za kiuchumi na kuchangia kikamilifu katika kukuza pato la Taifa.

Post a Comment

0 Comments