VIONGOZI WA AFRIKA WAMPONGEZA MUSEVENI BAADA YA KUSHINDA UCHAGUZI WA URAIS UGANDA

Viongozi mbalimbali barani Afrika wamejitokeza kumpongeza Rais mteule wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, kufuatia kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika nchini humo. Ushindi huo unaashiria kuanza kwa muhula wake wa saba madarakani.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, Museveni mwenye umri wa miaka 81 alipata asilimia 71.65 ya kura katika uchaguzi uliofanyika Alhamisi, Januari 15, 2026, akimshinda mpinzani wake wa karibu, kiongozi wa upinzani Bobi Wine, aliyepata asilimia 24.72 ya kura.

Ushindi huo unamthibitisha Museveni kama mmoja wa viongozi waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, tangu alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1986.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kumpongeza Museveni, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

“Hongera Rais @KagutaMuseveni kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Uganda,” alisema Kagame. “Nakupongeza wewe na wananchi wa Uganda mnapoendelea kulitumikia taifa lenu kwa ustawi wa watu wenu. Natarajia kuendelea kwa ushirikiano imara na wenye tija kati ya nchi zetu mbili.”

Kwa upande wake, Rais wa Kenya William Ruto ameuelezea ushindi wa Museveni kama kielelezo cha uaminifu wa umma kwa uongozi wake.

“Ushindi wako thabiti katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni unaonyesha imani ambayo wananchi wa Uganda wanayo kwa uongozi wako binafsi pamoja na uaminifu wao kwa chama cha NRM,” alisema Ruto.

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, naye alimpongeza Museveni, akihusisha ushindi huo na mchango wa Uganda katika kudumisha utulivu wa kikanda.

“Chini ya uongozi wake, Uganda imepiga hatua kubwa katika maendeleo na utulivu wa kikanda,” alisema, akiongeza kuwa Somalia itaendelea kuimarisha uhusiano wa karibu na Uganda.

Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) pia ilitoa pongezi zake, ambapo Mwenyekiti wake, Mahmoud Ali Youssouf, alisifu namna uchaguzi ulivyofanyika.

“Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika anasifu jinsi uchaguzi ulivyofanyika Uganda na anampongeza Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni kwa kuchaguliwa tena kwa asilimia 71.61 ya kura,” ilieleza AU katika taarifa yake baada ya uchaguzi wa Januari 15.

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, aliutaja ushindi wa Museveni kuwa ni “ushindi mkubwa” na kuonesha nia ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa pande mbili kati ya nchi hizo.

“Wananchi wa Jamhuri ya Uganda wamekukabidhi tena uongozi kwa kukuchagua kwa muhula wa saba,” alisema Kiir. “Natarajia kufanya kazi kwa karibu nawe ili kukuza zaidi uhusiano wa pande mbili.”

Naye Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi, alimpongeza Museveni kwa kuchaguliwa tena, akieleza kuwa matokeo hayo yanaakisi imani ya wananchi wa Uganda kwa uongozi wake.

“Ninatoa pongezi zangu kwa kaka yangu na rafiki, Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta Museveni, kufuatia kuchaguliwa kwake tena,” alisema el-Sisi, akiongeza kuwa matokeo hayo yanaonesha “imani ya watu wa Uganda kwa uongozi wake wenye busara.”

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Museveni alisema matokeo hayo yanaonesha uungwaji mkono wa dhati kwa chama chake licha ya kiwango kidogo cha ushiriki wa wapiga kura. Alieleza kuwa asilimia 52 ya wapiga kura walijitokeza, ikiwa ni kiwango cha chini zaidi tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini humo mwaka 2006.

“Matokeo haya yanaonesha wazi nguvu ya chama chetu. Upinzani wana bahati; hawajawahi kuona nguvu yetu kamili,” alisema Museveni.

Hata hivyo, uchaguzi huo uligubikwa na utata, baada ya mamlaka kusitisha huduma za mtandao kwa siku kadhaa, pamoja na hitilafu za mashine za kutambua wapiga kura kwa njia ya bayometriki, hali iliyosababisha ucheleweshaji wa upigaji kura katika baadhi ya maeneo, ikiwemo mji mkuu Kampala.

Kwa upande wake, Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 43 na ambaye awali alikuwa mwanamuziki kabla ya kuingia katika siasa, alisema alilazimika kujificha baada ya vikosi vya usalama kuvamia nyumbani kwake mara baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.

Bobi Wine amepinga matokeo ya uchaguzi huo akidai kuwa ni batili kutokana na tuhuma za wizi wa kura. Serikali ya Uganda imekanusha madai hayo na kumtuhumu kiongozi huyo wa upinzani kwa kuhamasisha wafuasi wake kufanya vurugu.

Post a Comment

0 Comments