Anwani za Makazi ZATAJWA KUIMARISHA USIMAMIZI WA MAZINGIRA – NEMC

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kutoa elimu kwa wananchi katika Kongamano la Mwaka la Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia ya Huduma za Posta 2026, linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo, linalotarajiwa kufungwa Februari 8, 2026, limewakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia, huduma za posta, pamoja na umuhimu wa usimamizi bora wa mazingira.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mhandisi Mkuu wa NEMC, Bw. Jampyon Mbugi, amesema matumizi sahihi ya anwani za makazi yana mchango mkubwa katika kupanga makazi, kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kurahisisha upatikanaji wa taarifa kupitia mfumo wa NAPA.

Ameongeza kuwa NEMC inalenga kuwajengea wananchi uelewa wa wajibu wao wa kisheria na kijamii katika kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Naye Mhandisi wa Migodi wa NEMC, Bw. Hezron Mwashibanda, amesema banda la NEMC katika kongamano hilo linatoa huduma mbalimbali ikiwemo ushauri wa mazingira, udhibiti wa kelele, ufuatiliaji wa TAM/EIA pamoja na utozaji wa ada na tozo za mazingira.

NEMC imewahimiza wananchi, wawekezaji na wadau wa maendeleo kutembelea banda lao ili kujifunza zaidi kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments